Ijumaa 18 Septemba 2026 - 19:30
Wanazuoni wa Umma wa Kiislamu Wanapaswa Kuchukua Msimamo Mmoja Dhidi ya Dhuluma

Hawzah/ Sheikh Muhammad Qadura, Rais wa Kituo cha Badr al-Kubra cha Palestina, akisisitiza umuhimu wa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, ametoa wito kwa Waislamu na wanazuoni wa Umma kuchukua msimamo wa pamoja dhidi ya dhuluma na uchokozi.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Muhammad Qadura, Rais wa Kituo cha Badr al-Kubra cha Palestina, katika kikao cha kwanza cha kimataifa cha “Ba’thatu Ummati Muhammad”, kilichofanyika Jumatano, tarehe 25 Shahrivar 1405 (Sep 16 2026), kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, alisisitiza umuhimu wa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu na kutoa wito kwa Waislamu na wanazuoni wa Umma kuchukua msimamo wa pamoja dhidi ya dhuluma na uchokozi.

Akinukuu aya za Qur’ani:

«وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِیعًا وَلَا تَفَرَّقُوا»

na

«وَإِنَّ هَذِهِ أُمَّتُکُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّکُمْ فَاعْبُدُونِ»

Alisema: Umma wa Kiislamu unapaswa kusimama kama mkono mmoja mbele ya dhuluma na uchokozi, hususan kile alichokiita kuwa ni vitendo vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya mataifa ya eneo hili.

Qadura, akizungumzia msimamo wa Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuhusu matukio ya Ulimwengu wa Kiislamu, alisema: Katika miaka iliyopita, amekuwa akichukua msimamo dhidi ya uchokozi na dhuluma zinazofanywa dhidi ya mataifa mbalimbali, yakiwemo Palestina, Lebanon, Yemen, Iraq na Afghanistan, na amesisitiza umuhimu wa kukabiliana na dhuluma.

Rais wa Kituo cha Badr al-Kubra cha Palestina aliongeza: Kuunga mkono waliodhulumiwa hakupaswi kuwa jambo linalomhusu mtu mmoja, kiongozi mmoja au mtawala mmoja pekee, bali ni wajibu wa jumla, na Umma wote unapaswa kuchukua msimamo dhidi ya dhuluma.

Alisisitiza: Kukabiliana na dhuluma na ubeberu ni wajibu wa kibinadamu na kimaadili, na hakupaswi kufungamanishwa na dini, utaifa au nafasi ya kisiasa ya watu; Waislamu wanapaswa kumuunga mkono anayeadhulumiwa popote pale dhuluma inapotokea.

Qadura aliendelea kwa kuzungumzia hali ya Ghaza, na kukosoa kile alichokiita kuwa ni ukimya au mwitikio usiotosheleza wa baadhi ya wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu kuhusu matukio katika eneo hilo. Alisema: Wanazuoni wa Umma wanapaswa, kama walivyowahi kuchukua hatua katika vipindi mbalimbali kuhusiana na migogoro na mapigano katika baadhi ya nchi za Kiislamu, pia kuchukua msimamo ulio wazi dhidi ya mateso ya wananchi wa Ghaza.

Akizungumza na wanazuoni wa Ulimwengu wa Kiislamu, alisema: Leo tunahitaji umoja na uratibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote, na wanazuoni wanapaswa kusimama kwa sauti moja dhidi ya dhuluma na ubeberu.

Rais wa Kituo cha Badr al-Kubra cha Palestina pia alisisitiza: Kupinga dhuluma kunapaswa kufanywa bila kujali utambulisho au kaulimbiu ya dhalimu, na iwapo mtu au kundi fulani, licha ya kujinasibisha na Uislamu, litafanya dhuluma, Waislamu hawapaswi kunyamaza mbele ya vitendo vyake vya kidhalimu.

Qadura alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa Umma wa Kiislamu kurejea katika mafundisho ya Qur’ani Tukufu na mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), akisema: Umoja wa Kiislamu unapaswa kutekelezwa katika jamii kwa maana yake halisi; umoja ambao utapelekea mataifa kuwa karibu na siyo kusababisha mgawanyiko. Alieleza matumaini yake kwamba wito huu utafika katika masikio ya dhamiri zilizo hai za Ulimwengu wa Kiislamu, na kwamba Waislamu watarudi katika njia ya umoja, uelewa na kutekeleza wajibu wao wa kidini na kibinadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha